Wakaazi zaidi ya 1,500 kutoka wadi ya Keringet katika eneo bunge la Kuresoi Kusini wanatarajiwa kunufaika na maji masafi ya kunywa yatakayoletwa na mradi wa maji wa Soitaran ambao unapangwa kuanza wiki hii.
Mradi huu wa maji, unaoendeshwa na Serikali ya Kaunti ya Nakuru, unanuiwa kuhakikisha kuwa wakaazi wanatumia maji masafi nyumbani mwao na pia kwa maslahi ya ufugaji; hali ambayo itawawezesha kujiepusha na maradhi yanayosababishwa kwa kutumia maji machafu.
Afisa wa Maji wa eneo hilo, James Tirop, amesema maji ni muhimu sana katika maisha ya binadamu na hivyo basi akawaomba wakaazi kuitumia rasilimali hii vyema pindi tu mradi huu utakapokamilika ili kuwanufaisha muda mrefu.
Aidha aliongeza kwamba wakaazi watapata muda wa kushughulikia mambo mengine kadha wa kadha kwa kuwa wako na maji safi manyumbani mwao kinyume na ilivyokuwa hapo awali ambapo walitembea kilomita tatu ili kuchota maji safi.